WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameonya tabia ya wasimamizi wa misitu kuingia mikataba binafsi na wamiliki wa mifugo hasa ng'ombe kulisha katika hifadhi za misitu nchini.
Amesema kitendo hicho kimesababisha kuharibika kwa uoto wa asili na kuleta uharibifu mkubwa katika hifadhi za misitu.
Akizungumza katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Misitu nchini (TFS) mjini Dodoma, Profesa Maghembe amesema misitu nchini ipo hatarini kutoweka kutokana na uamuzi binafsi unaofanywa na watu wenye dhamana ya kutunza misitu.
Amesema wanyama wanaoingizwa ndani ya misitu wakiwemo ng'ombe, mbuzi na kondoo wanavuruga utaratibu wa asili na kuua vyanzo vya maji, hivyo kuleta ukame.
Waziri Maghembe amesema hifadhi ya misitu mingi kwa sasa imekuwa ni kama shamba la bibi kutokana na kila mtu kuamua kuitumia kwa shughuli zake binafsi ikiwamo ukataji magogo, utengenezaji wa mkaa na kuingiza mifugo.
Amesema anachukizwa kwa kuteketea kwa misitu huku maofisa wasimamizi wapo na wao wakibaki kuwa sehemu ya malalamiko.
Amesema japokuwa kuna matatizo ya wakala wa misitu ikiwamo ya upungufu wa vitendea kazi pamoja na masuala ya utawala huku wakiwa na wajibu wa kutunza rasilimali za misitu, kasi ya uharibifu wa misitu ni lazima isimamishwe.
No comments:
Post a Comment