Antonio Conte anaamini Nathan Ake anaweza kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Chelsea duru la pili Ligi Kuu Uingereza msimu huu
Beki Ake ameitwa kutoka Bournemouth alipokuwa akitumika kwa mkopo mwezi huu baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika kikosi cha Eddie Howe.
Na Conte amesisitiza kuwa Mdachi huyo amerejeshwa klabuni mwake dirisha la uhamisho Januari si kwa ajili ya matakwa ya kifedha kwa kutaka kumuuza, la!
Badala yake, Muitaliano huyo anaamini Ake kama mchezaji mahiri atakuwa mchezaji muhimu kuisaidia Chelsea kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi na hata kutwaa taji.
“Nathan Ake amerudi kwenye kikosi chetu kwa sababu nimethaminisha hali yake na hali yetu na anaonekana kuwa na ari,” Conte aliwaambia waandishi kwenye mkutano.
“Ake ni mchezaji anayeweza kucheza kwenye nafasi tofauti-tofauti. Nadhani ameimarika sana na sasa yupo tayari kucheza kwenye kikosi cha Chelsea na atatusaidia.
“Hii ni wiki ya pili amekuwa nasi na ameanza kuelewa falsafa yetu ya mpira. Napendezwa naye.”
Jumapili Chelsea watawakabili Hull City ambao wapo kwenye kipindi kigumu Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment