Friday, November 11, 2016

SITTA AIBUA HOJA YA "BUNGE LIVE" MWILI WAKE UKIAGWA DODOMA LEO


Image result for picha za mwili wa sitta
Askari wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu, Samuel Sitta baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana. 
 Shughuli za kuaga mwili wa Spika wa Bunge mstaafu Samuel Sitta aliyefariki dunia nchini Ujerumani, leo zitarejesha taratibu wa Bunge kurushwa moja kwa moja (live) kwa kuwa ndiye aliyeasisi utaratibu huo.

Tokea Januari mwaka huu, Bunge la 11 lilizuia kurusha matangazo ya shughuli zake moja kwa moja kwa madai kuwa ni gharama kubwa kufanya hivyo.

Hivi sasa shughuli za Bunge zinazoonyeshwa moja kwa moja ni maswali na majibu na hotuba za mawaziri wakati wa bajeti kuu.

Spika wa Bunge, Job Ndugai jana alitangaza bungeni mara baada ya kuwatambulisha wageni kuwa shughuli hizo zitarushwa moja kwa moja na vyombo vya habari hatua iyolenga katika kumuenzi muasisi wa utaratibu wa kurusha shughuli za Bunge moja kwa moja.

“Kikao hiki maalumu kitakuwa ‘live coverage’ (matangazo ya moja kwa moja) mtindo ambao ulianzishwa chini ya uongozi wake Spika wa kasi na viwango,” alisema Spika Ndugai huku akifunga vifungo vya joho lake la kuongozea Bunge.

Sitta licha ya kuwa mwanzilishi wa Bunge Live, pia alianzisha utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kila siku ya Alhamisi wakati Bunge linapokuwa na mkutano wake, pia utaratibu wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali kuongozwa na wabunge kutoka kambi ya upinzani.


Ndugai alisema wabunge wataupokea mwili wa Sitta kwenye Uwanja wa Ndege wa Dodoma, leo saa 8:00 mchana.

Alisema wabunge wote wanatakiwa kuwa wameketi ndani ya Ukumbi wa Bunge tayari kwa kikao hicho maalumu cha Bunge cha kihistoria kitakachoanza saa 8:30 mchana.

Alisema jeneza lenye mwili wa Sitta litawekwa mbele ya kiti cha Spika ndani ya ukumbi huo na kwamba wabunge watatoa salamu za rambirambi.

Spika alisema wabunge wote wataaga mwili huo, ingawa jenezahalitafunguliwa na kuwa shughuli zote za kuaga mwili huo zitafanyika kwa muda wa saa mbili walizopewa.

“Hatua hii itajenga msingi kwa Taifa ambapo viongozi wa kitaifa watakapofariki dunia, miili yao itakuwa ikiagwa kwenye Ukumbi wa Bunge ambako wawakilishi wa Watanzania wote wanapatikana badala ya kwenye Uwanja wa Taifa (jijini Dar es Salaam) na maeneo mengine,” alisema.

Ndugai alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe wataongoza katika utoaji wa salamu za rambirambi kwa wabunge.

Alisema baada ya shughuli hiyo jeneza lenye mwili wa Sitta litatolewa nje ya ukumbi huo ili kutoa nafasi ya kutolewa hoja ya kuahirishwa kwa Bunge.

Alisema baada ya kuahirishwa kwa Bunge, wabunge watajipanga nje ya ukumbi huo na kupokezana jeneza hilo hadi kwenye gari litakaloupeleka mwili huo Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ajili ya kusafirishwa kuelekea Urambo mkoani Tabora kwa ajili ya maziko.

Hata hivyo, alisema wabunge 10 ambao watateuliwa na Tume ya Utumishi ya Bunge kwa uwiano wa vyama watawakilisha Bunge katika shughuli za maziko hayo.

Alisema ujumbe huo utaongozwa na yeye mwenyewe (Ndugai) ambao utaondoka kesho (Jumamosi) na kurejea siku hiyo hiyo mjini Dodoma.

Ili kufanikisha kwa shughuli hiyo aliyoiita ya kihistoria, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama alitengua vifungu vya kanuni ili kuruhusu mwili na baadhi ya ndugu wa marehemu kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.

Kanuni za Bunge zilizotenguliwa ili kuruhusu shughuli hiyo ni ni 139 (1), 143 (e) – (f) na 143 ili kuwezesha ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu wasiozidi 12 na jeneza lililobeba mwili wa Sitta kuingia ndani ya ukumbi huo.



Samia aongoza waombolezaji

Wakati huohuo; Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan jana aliongoza mamia ya waombolezaji waliofika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kuupokea mwili wa Spika Sitta baada ya kuwasili ukitokea nchini Ujerumani alikofariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya tezi dume.

Mwili wake uliwasili usaa 9:00 jioni kwa Shirika la Ndege la Emirates na kupelekwa nyumbani kwake Masaki Kinondoni ambako utalala.

Simanzi zilitawala uwanjani hapo baada ya Samia kumpokea mjane wa marehemu, Margareth Sitta ambaye alikuwa akimuuguza nchini humo.

Viongozi wengine waliofika kuupokea mwili huo ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi na Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi.

Wengine ni Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na baadhi ya mawaziri.

Leo asubuhi mwili wa Sitta utaagwa katika Viwanja vya Karimjee na viongozi mbalimbali wa kitaifa na dini na mchana utaagwa na wabunge mjini Dodoma.

Jumamosi mwili wa Sitta utazikwa wilayani Urambo baada ya kuagwa na ndugu, jamaa na marafiki.

Akizungumza uwanjani hapo, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye alikuwapo alisema Taifa limempoteza Sitta ambaye alikuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi. “Nimempoteza kaka yangu na kiongozi ambaye alikuwa mfano wa kuigwa katika nyadhifa alizozishika katika nchi hii,” alisema.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema Sitta atakumbukwa kwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.

Alisema mfuko huo ulianzishwa ili kuwawezesha wabunge kuwaletea wananchi maendeleo bila kutegemea fedha za kuomba kutoka kwa matajiri.

No comments:

Post a Comment