YANGA SC imevunja mwiko wa kutoshinda Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kwa miaka 30 baada ya jioni ya leo kuwafunga Maji Maji 1-0 kwenye Uwanja huo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ushindi huo unawafanya mabingwa hao watetezi, Yanga wafikishe pointi 43 baada ya kucheza mechi 19, ingawa inaendelea kukaa nafasi ya pili nyuma ya vinara Simba SC wenye pointi 44 za mechi 18.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hussein Athumani aliyesaidiwa na Mirambo Tshikungu na Vincent Mlabu, hadi mapumziko Yanga walikuwa tayari mbele kwa bao hilo moja.
Baada ya bao hilo, Maji Maji nao wakafunguka na kuanza kushambulia moja kwa moja langoni mwa Yanga, lakini safu ya ulinzi ya wana Jangwani iliyoongozwa na nguli Kevin Yondan ilisimama imara kudhibiti hatari zote.
Yanga ingeweza kumaliza kipindi cha kwanza inaongoza kwa mabao zaidi kama ingetumia vizuri nafasi zaidi, ikiwemo ile ya dakika ya pili tu baada ya kiungo Juma Mahadhi kujigonga gonga na mpira miguuni baada ya pasi nzuri ya mshambuliaji Amissi Tambwe kwenye boksi hadi beki Keneddy Kipepe akaokoa na kuwa kona iliyookolewa pia.
Mapema dakika ya 25, kocha wa Maji Maji na mchezaji wa zamani wa Yanga, Kali Ongala alimtoa beki Bahati Yussuf na kumuingiza Emmanuel Semwanza aliyesajiliwa dirisha dogo Desemba kwa mkopo kutoka Maji Maji.
Na mwanzoni tu mwa kipindi cha pili, Ongala mtoto wa gwiji wa zamani wa muziki nchini, Dk. Remmy Ongala (sasa marehemu) akamuingiza Peter Mapunda kwenda kuchukua nafasi ya Lucas Kikoti.
Mabadiliko hayo, hayakuweza kuwasaidia Maji Maji, kwani pamoja na kupeleka mashambulizi mengi kwenye eneo la Yanga, hawakuchomoa bao.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa michezo miwili, Simba wakiwa wageni wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Azam FC wakiwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment