Friday, August 19, 2016

YANGA YAPANIA KULIPA KISASI DHIDI YA TP MAZEMBE


Timu ya Yanga baada ya kupoteza mechi ya Ngao ya Jamii kwa Azam FC sasa inatarajiwa kwenda DR Congo kulipa kisasi kwa TP Mazembe
Baada ya juzi kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii kwa penati 4-1, kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini Jumamosi kuelekea DR Congo kwa ajili ya mchezo wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe.
Meneja wa Yanga Baraka Desidedit ameiambia DSS TV , maandalizi yote kwa ajili ya safari hiyo yanakwenda vizuri na timu yao baada ya mchezo wa jana itafanya mazoezi kesho Ijumaa na Jumamosi baada ya mazoezi wataondoka kuelekea Congo.
“Ni mchezo ambao tumejipanga kupata ushindi hata kama hatuna nafasi ya kusonga mbele tunachotaka kulipa kisasi baada ya kutufunga kwenye mchezo wa kwanza hapa nyumbani,” amesema Baraka.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi Helder Martins De Carvalho wa Angola, atakayesaidiwa na washika vibendera Jean Claude Birumushashu wa Burundi na Arsenio Chadreque Marengula wa Msumbiji.
Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi tano na imekwishafuzu nusu fainali, ikifuatiwa na Medeama yenye pointi nane, Mouloudia Olympique Bejaia pointi tano na Yanga inayoshika mkia kwa pointi zake nne. 

No comments:

Post a Comment